KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ameonekana kukoshwa na idadi kubwa ya mashabiki wa soka wanaojitokeza mikoani, akisema imekuwa chachu ya wachezaji wake kucheza kwa kujituma na kupata ushindi kwa asilimia 100 kwenye michezo ya ugenini ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo imekuwa kama ipo nyumbani.
Akizungumza jijini Dodoma , ambako timu hiyo imeweka kambi ya muda kabla ya kuivaa Fountain Gate, katika mechi ya raundi ya 17 ya Ligi Kuu itakayopigwa kesho, Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, kocha huyo alisema ameshangazwa na idadi kubwa ya mashabiki wanavyojitokeza kwenye viwanja vya mikoani, na cha ajabu zaidi ni kwamba zaidi ya asilimia 90 wamekuwa wakiishangilia Simba kwa nguvu zote, kitu ambacho kinamfanya yeye na wachezaji wake kufanya kila juhudi kuhakikisha wanaondoka uwanjani na furaha baada ya mchezo.
"Nimeona kwenye michezo mingi mikoani, kumekuwa na mashabiki wengi uwanjani na wanakuwa wanatushangilia sisi, kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mashabiki walitia fora, walijitokeza kwa wingi zaidi, uwanja ulijaa sana, na karibuni wote walikuwa upande wetu, utagundua hilo bao linapofungwa, uwanja mzima unasimama kushangilia, tulikuwa ugenini, lakini ni kama nyumbani tu, hili pamoja na mambo mengine ya ufundi na mifumo, lakini nalo kiasi kikubwa linatusukuma sana kupata ushindi," alisema.
Simba imeshinda mechi zote nane ilizocheza ugenini mpaka sasa, ikiwa kinara wa kushinda mechi nyingi za ugenini mpaka sasa.
SOURCE: IPP

EmoticonEmoticon