LICHA ya kuwepo na
tetesi zinazomuhusisha nyota wa Real Madrid Cristiano Ronaldo kuwa anaweza
kuitema klabu hiyo na hivyo kuwa pigo kubwa kwao, lakini staa wa zamani Luis
Figo ameibuka akisema kuwa hakuna mtu ambaye pengo lake haliwezi kuzibika na
hivyo akiondoka poa tu.
Hadi sasa bado Ronaldo hajaweka wazi kuhusu hatma yake
baada ya wiki iliyopita kudaiwa kuwa anaweza kuitema klabu hiyo ya Santiago
Bernabeu. Kutokana na kile ambacho inadaiwa kuwa haimlindi katika sakata lake
la ukwepaji kodi ya kiasi cha pauni mil 13. Kutokana na sekeseke hilo, klabu
yake ya zamani ya Manchester United na Paris Saint Germain ndizo zinazotajwa
kuwa huenda staa huyo mwenye umri wa miaka 32 akakimbilia huko.
Pamoja na
taarifa hizo, mapema wiki hii rais wa Real Madrid, Florentino Perez alisema
kuwa hawana mpango wa kuiuza hazina yao hiyo kuu lakini Figo anaonekana
kupingana nae baada ya kusema hakuna mchezaji ama mkurugenzi ambaye anaweza
kuwa mkubwa wakati anapojiunga na mabingwa hao wa La Liga na Ulaya.
“Haya ni
maoni yangu kwamba hakuna mchezaji ambaye nafasi yake haizibiki na hata kama
akiwa ni Cristiano Ronaldo,” Figo aliuambia mtandao wa Goal wakati alipoulizwa
kuhusu hatma ya straika huyo wa Ureno. “Klabu haiwezi kumtegemea mtu mmoja,
historia ya klabu kama hii iko juu ya kila mmoja, hata awe mkurugenzi ama mtu
gani,” aliongeza staa huyo wa zamani.
Mbali na hilo alisema kuwa licha ya
wengine kudai kuwa Real Madrid haitaweza kufanya vyema bila ya Ronaldo lakini
Figo anasema kuwa hilo halimuingii kichwani kama mshindi huyo wa tuzo ya 2016
Ballon d’Or ambaye anapewa nafasi ya kuinyakuwa tena mwaka huu anaweza kuondoka.

EmoticonEmoticon