BAYERN MUNICH imezionya klabu pinzani kuacha kumshawishi
mshambuliaji wao Robert Lewandowski, na itakayopuuza ijiandae kupata vikwazo
kutoka Fifa. Staa huyo raia wa Poland amekuwa akihusishwa na uhamisho kwenda
Chelsea au Manchester United, na ripoti zinadai kuwa tayari mazungumzo ya awali
kuhusu dili hilo yameanza.
Hata hivyo Bayern imetoa taarifa kukanusha madai
hayo ikisema: “Robert ana mkataba na Bayern na ni hivi karibuni tu ameurefusha
hadi 2021. Bayern Munich haitapoteza muda kuwaza juu ya uhamisho wa
Lewandowski. “Hakuna mazungumzo na klabu nyingine na hakutakuwa na mazungumzo
na klabu yoyote.
Kama klabu nyingine zitafanya makubaliano na wachezaji ambao
wapo kwenye mikataba ya muda mrefu, zina hatari ya kuadhibiwa na Fifa. Wakala
pia ametuthibitishia kwamba hajafanya mazungumzo yoyote ya mkataba.” Kwa upande
mwingine hali inaonekana haiko sawa kwa Lewandowski baada ya wakala wake, Maik
Barthel, kuikosoa Bayern kwa kutomsaidia mteja wake kushinda kiatu cha dhahabu.
Straika huyo alifunga mabao 30 msimu uliomalizika na alihitaji kufunga mara
mbili katika mechi ya mwisho dhidi ya Freiburg waliyoshinda 4-1 kuweza kumpiku
Pierre-Emerick Aubameyang wa Borussia Dortmund aliyeibuka kinara. “Robert
aliniambia hakupata sapoti na kwamba kocha hakumpigia simu kumsaidia katika
mechi ya mwisho ili ashinde taji la mfungaji bora. Alikatishwa tamaa, sijawahi
kumwona kabla. Alikuwa na matumaini kwamba timu ingeweza kumsaidia kufanikisha
kwa ufanisi,” Barthel aliliambia gazeti la Kicker.

EmoticonEmoticon